Waziri wa Nchi Afisi ya Rais, Kazi, Uchumi na Uwekezaji Mhe. Shariff Ali Shariff amefungua mafunzo maalum kwa viongozi wa Afisi hiyo yaliyoandaliwa na Chuo cha Utawala wa Umma - IPA katika Ukumbi wa ZIPA uliopo Wilaya ya Magharibi A. Mhe. shariff amesema mafunzo hayo yatawasaidia viongozi wa Afisi hiyo kuweza kujitambua na kuweza kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi zaidi.
Ameushukuru uongozi wa chuo hicho kwa kuandaa mafunzo hayo ya kuwajengea uwezo viongozi hao ambayo yatawawezesha kufanya vyema kazi zao na amewaomba mafunzo hayo kuwa endelevu.
Hata hivyo, amewataka Makatibu Wakuu wa Afisi yake kuandaa utaratibu maalum wa kuwapatia mafunzo wafanyakazi wake hasa wale wa kada ya chini hatua ambayo itasaidia kuleta mabadiliko katika utendaji wao wa kazi.
Aidha, amewataka watendaji wa Chuo cha Utawala wa Umma kuandaa mapema utaratibu wa utoaji wa mafunzo kwa wafanyakazi wanaotarajiwa kustaafu ili yaweze kuwasaidia vyema mara baada ya kustaafu.
Katibu Mkuu anaeshughulikia masuala ya Kazi na Uwezeshaji Bi Maryam Juma Abdulla amesema mafunzo hayo yatawasaidia sana katika kutekeleza majukumu yao hasa katika suala la kuzingatia muda katika kutekeleza majukumu yao pamoja na kuweza kufanya kazi kwa mashirikiano baina ya viongozi na wafanyakazi.
Akiwasilisha mada ya mabadiliko katika uongozi na uzingatiaji wa muda katika kazi na wajibu wa pamoja katika Sekta ya Umma Katibu Mkuu Kiongozi Mstaafu ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Chuo cha Utawala wa Umma Dkt Abdulhamid Yahya Mzee ameesema ni jambo muhimu kwa kila mtumishi wa umma kufahamu wajibu wake na kufanya kazi kwa kuzongatia Sheria zilizopo.
Wakitoa michango yao baadhi ya washiriki wa mafunzo hayo wamesema wako tayari kuendelea kufuata sheria na miongozo ya kazi hatua ambayo itasaidia kuondosha baadhi ya malalamiko na matatizo yanayojitikeza katika sehemu za kazi pamoja na kuwa na ushirikiano mzuri baina ya viongozi ndani ya Taasisi