Waziri wa Nchi Afisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Mhe. Sharif Ali Shariff amewataka wafanyakazi kubadilika na kufanya kazi kwa kuzingatia misingi sheria na taratibu za kazi zinavyo elekeza hatua ambayo itasaidia kuongeza ufanisi katika sehemu za kazi.
Mhe. Shariff ameyasema hayo katika hafla ya makabidhiano ya Afisi kwa Makatibu Wakuu na na Manaibu Katibu Wakuu wapya wa Afisi hiyo walioteuliwa hivi karibuni na Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi.
Amesema kufanya hivyo kutaweza kusaidia Serikali na kuendana na kasi ya Serikali ya awamu ya nane ambayo ina lengo la kuwawezesha na kuwasaidia wananchi kupata huduma zote muhimu zinazotolewa katika taasisi.
Akizungumza baada ya kufanya makabidhiano hayo Katibu Mkuu Wizara ya Afya Dkt Habiba Hassan Omar amesema amemshukuru Rais kwa kuendelea kumuamini na kumteua ili andelee na majukumu yake katika Afisi hiyo na kuahidi kufanya kazi kwa mashirikiano ya pamoja kwa lengo la kufanikisha malengo ya Serikali ya kutoa huduma bora kwa wananchi .
Hata hiyo amewasisitiza viongozi wapya walio teuliwa katika Afisi hiyo kuendelea kufanya kazi kwa maendeleo ya nchi na taifa kwa ujumla.
Nao baadhi ya viongozi wapya walio teuliwa na kukabidhiwa majukumu yao akiwemo Katibu Mkuu (Uchumi na Uwekezaji) ndugu Khamis Suleiman Mwalim amesema wapo tayari kufanya kazi kwa mashirikiano ya pamoja na kufuata muongozo iliyopo ili kufanikisha maagizo na malengo ya Mhe. Rais katika Afisi hiyo.
Nae Katibu Mkuu (kazi na Uwezeshaji) Bi Maryam Juma Abdulla amewataka watendaji wote wa Afisi yake kubadilika na kuachana na tabia ya kufanya kazi kwa mazoea kwa maslahi mapana ya Taifa.