Katibu Mkuu anaeshughulikia Masuala ya Kazi na Uwezeshaji Afisi ya Rais , Kazi, Uchumi na Uwekezaji ndugu Maryam Juma Abdulla amevitaka vyama vya ushirika kuendelea kushirikiana na kuziondoa changamoto zilizopo ndani ya vyama hivyo ili viweze kuleta tija na maslahi kwao na taifa kwa ujumla.
Ushauri huo ameutoa katika mkutano wa wadau wa vyama vya ushirika wenye lengo la kujadili kuhusu utafiti wa hali ya ushirika Zanzibar kilichowashirikisha watendaji wa idara ya Maendeleo ya Ushirika na Watendaji wa Chuo cha Ushirika Moshi kilichofanyika huko Afisini kwake Mwanakwerekwe tarehe 17/07/2024.
Amesema vyama hivo vimekuwa vikikabiliwa na changamoto mbali mbali ikiwemo kutokuwa na elimu ya usimamizi mzuri wa fedha za wananchama, kutofata kanuni, katiba, na miongozo, kutokuwepo kwa utaratibu mzuri wa kuhifadhi kumbukumbu pamoja na kutokuwa na muundo wa aina moja katika vyama hivyo.
Aidha akizungumzia kuhusu utafiti huo Katibu Maryam amewataka wadau wa utafiti huo wahakikishe unalenga katika kuangalia matokeo ya mikopo iliyotolewa na Serikali kwa namna ambayo imeweza kuwasaidia wajasiriamali nchini.
Akiwasilisha andiko la utafiti huo Mhadhiri Muandamizi kutoka Chuo Cha Ushirika Moshi Bw Victoria Shirima amesema utafiti huo utalenga zaidi katika kutathimini uwezo wa vyama vya ushirika katika kukidhi mahitaji ya wananchama wa Zanzibar pamoja na kuangalia rasilimali zilizopo ndani ya vyama hivo.
Mkurugenzi Idara ya Maendeleo ya Ushirika ndugu Khamis Daud Simba amesema idara yake imejipanga kuwapa elimu wanachama wapya kuhusu umuhimu wa ushirika pamoja na kuwapa ushauri wa kutatua migogoro inapotokea katika vyama hivo.
Amesema Idara tayari imeanza kufanya utafiti wenye lengo la kuviletea mageuzi vyama hivo ili viweze kutoa huduma bora kwa wananchama wake.