Kamishna wa Kazi kutoka Kamisheni ya Kazi ndugu Rashid Othman amesema ni vyema kwa Taasisi za Serikali na binafsi kufuata sheria za kazi ipasavyo kwa lengo la kuleta ufanisi katika maeneo ya kazi.
Ameyasema hayo huko Afisini Mwanakwerekwe wakati wa kikao cha mafunzo ya kanuni mpya za Sheria ya Kazi kwa wadau mbalimbali wa masuala ya Kazi tarehe 15/08/2024.
Kamishna Rashid, amesema kanuni hizo zinatoa ufafanuzi pamoja na kuondoa changamoto mbalimbali zilizopo katika maeneo ya kazi.
Aidha, amesema kanuni hizo hazina lengo la kutoa adhabu kwa waaajiri bali zimewekwa kwa kuwalinda pamoja kuwakinga waajiriwa
Akiwasilisha kanuni ya kuchukua wanafunzi wa vitendo ya mwaka 2023 Afisa Kazi ndugu Khatib Khalid Hamad amesema lengo la kuanzishwa kwa kanuni hiyo ni kuondoa tatizo la utumikishwaji holela na malipo nafuu kwa wanafunzi hao bila ya kuzingatiwa ujira wa kazi pamoja na kuongeza fursa za ajira kwa vijana.
Nao wachangiaji wa kikao hicho wamesema bado kanuni hizo zinahitaji maboresho kwa lengo la kuleta ufanisi katika maeneo ya kazi.
Kanuni nyengine zilizowasilishwa ni pamoja na Kanuni ya maombi ya barua maalum ya utambuzi kwa wafanyakazi wa kigeni walio kwenye ndoa na Mzanzibari ya mwaka 2023 pamoja na Kanuni ya Kumaliza Makosa.