Watendaji wa Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji wametakiwa kuendelea kufanya kazi kwa ushirikiano ili kuleta ufanisi katika kazi zao za kila siku.
Ushauri huo umetolewa na aliyekuwa Katibu Mkuu (Kazi na Uwezeshaji)Bi Maryam Juma Abdulla ambae kwa sasa ni Katibu Mkuu Ofisi ya Makamo wa Kwanza wa Rais mara baada ya kukabidhi majukumu ya Ofisi hio kwa Katibu Mkuu wa sasa Ndugu Khamis Suleiman Mwalim yaliyofanyika huko ofisini Mwanakwerekwe Wilaya ya Magharib B tarehe 26�82024
Makabidhiano hayo yamefanyika kufuatia uteuzi uliofanywa hivi karibuni na Mhe.Rais na Mwenyekiti wa baraza la Mapinduzi Zanzibar Dkt.Hussein Ali Mwinyi kwa Makatibu Wakuu. Bi Maryam amesema ni muhimu kuwa na mashirikiano ya pamoja kwa kufanya kazi kwa kujitolea na kumpa mashirikiano mema Katibu mpya wa Ofisi hiyo ili kuweza kufikia malengo waliyokusudiwa.
Aidha amewataka watendaji kuimarisha uwajibikaji kwa kuhakikisha utekelezaji wa malengo yanafikiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni za kazi pamoja na kufuata utaratibu mzuri wa kusimamia mapato yanayokusanywa kwa mujibu wa miongozo iliyopangwa. Katibu Maryam ameongezea kuwa watendaji hao wanatakiwa kuimarisha mashirikiano na wadau mbali mbali wa maendeleo pamoja na kuimarisha utoaji wa huduma bora kwa wananchi
Kwa upande wake Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Kazi Uchumi na Uwekezaji Ndugu Khamis Suleiman Mwalim ameahidi kushirikiana na watendaji wa Ofisi hiyo kwa kufanya kazi kwa bidii ili kuhakikisha malengo na maono ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar yanafikiwa.
Amesema ni muhimu kwa wafanyakazi kubadilika na kufanya kazi kwa kuzingatia sheria na miongozo ya utumishi wa umma kama zinavyotakiwa.
Aidha Katibu Khamis ameahidi kuendelea kuwapa mashirikiano mazuir watendaji wa Ofisi hiyo pamoja na kumshukuru Mheshimiwa Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Wawakilishi kwa kumteuwa na kumuamini katika utendaji wake wa kazi za Serikali.